4. Kisome kisa hiki kisha ujibu maswali maabaye.
Hivi majuzi vyombo vya habari viliibuka na kituko cha kuvunja mbavu. Ghulamu mmoja alijitokeza kazaliwa upya kageuka msichana! Sauti yake nyororo ya kike ilisikika kwa kuwatia wengi taharuki. Kijana huyu alikuwa akifanya kazi kama kijakazi katika familia mbalimbali. Waajiri wake waliokuwa siku zote hizo wakidhani kuwa ni banati, walimwacha kutumia chumba kimoja na wenzake.
Ujana wa ‘kipusa’ wetu ulipogunduliwa, hakuonekana kupigwa na mshipa. Kelele za watu waliokuwa wakitaka kumrambisha shubiri zilionekana kwake kama mkoromo wa chura ambao haumzuii ng’ombe kukata kiu yake. Cheche zote za matusi kutoka kwa waja ziliangukia masikio yenye nta kwani ‘banati’ huyu ambaye alikuwa kajitanda buibui kama kawaida ya jumuiya yake, alishikilia kuwa alikuwa na haki kulifanya alitakalo. Yamkini hakujua kuwa haki nayo ina mipaka.
Waajiri wengine hasa akina mama, walihadithia jinsi walivyomwamini kijakazi huyu mnyenyekevu kiasi cha kuachia chui mbuzi. Mmoja wao alisikika akilalamika kwamba ‘msichana’ huyu, kwa jina Mzaha alikuwa amewaadhiri wanawe wa kike vibaya kwa kuwashawishi wasiende shule. Aliwaelekeza watoto hawa kwa wanaume ambao alisema wangewapa pesa.Ingawa haikubainika kama kweli wana hawa walipelekwa ‘mawindoni’ hili ni wazo la kutisha na kuhuzunisha sana.
Watazamaji wengi wa runinga bila shaka walikilaani kitendo hicho. Hata hivyo, jambo la kujiuliza nje, kwa nini mvulana huyu akataka kua msichana bandia?
Visa vingi vya uhalifu na maovu ya kijamii vimetokea kwa sababu mbalimbali. Baadhi ya vijana wanadai kwamba kwa sababu ya uhaba wa kazi, hawana budi kufanya kazi yoyote il e, almuradi wapate riziki,japo ya siku moja. Huyu aliamua kuwa ‘kijakazi’ ili apate kazi katika nyumba za watu ambako ana hakika ya kupata mahitaji ya msingi kama vile malazi na chakula.
Ukosefu wa mawasiliano kati ya wazazi na wanao huenda likawa chanzo mojawapo ya matatizo ya watoto. Migogoro itokeapo, baadhi ya vijana huhiari kutorokea mijini na kufikwa na ya kuwafika.
Ni kweli kwamba jamii yetu imelemazwa na umaskini uliokithiri. Hata hivyo, hatupaswi kuchukulia maadili ya kijamii kuwa jambo la mzaha. Wale ambao wameona kuwa maisha ni kuendeleza ulaghai kama shamsha na wengine wengi wanapaswa kukumbuka kuwa tatizo halitatuliwi kwa tatizo lingine . Kwani kwa kufanya hivyo watajiingiza kwenye mafundo ambayo hawawezi kujitanzua kwayo. Vijana wahimizwe kujiunga na makundi kama yale ya kuzoa taka mjini ili kujiepusha na uhalifu. Wanaohitimu darasa la nane na kushindwa kuendelea na elimu wafunzwe kazi za kaufundi ili waweze kujiunga na kundi la jua kali. Kwa njia hii, wataweza kujikimu na kuzikimu aila zao. Shime! Tuhimize maadili.